BARUA YA WAZI KWA EMMANUEL, FLORA MBASHA

KWENU,
Emmanuel na Flora Mbasha. Naamini afya zenu zipo sawa na mnaendelea kuhangaika na maisha ingawa kuna changamoto zimeingia kati yenu. Napenda kuwahakikishia kuwa, hayo ni mapito tu. Yataisha.

Naandika barua hii hasa kwa msukumo wa imani yangu ambayo nanyi mnaiamini. Kwangu mimi kama Mkristo, ninyi ni viongozi wangu wa kiroho. Sina shaka na hilo hata kidogo.
Flora Mbasha akiwa na mumewe Emmanuel Mbasha.
Ni viongozi wa Wakristo wengi ndani na nje ya nchi. Nasema hivyo kwa sababu ninyi ni Wainjilisti, mnaotangaza neno kupita uimbaji! Mmebadilisha maisha ya wengi kwa kupitia nyimbo zenu.
Kwa msingi huo sina shaka yoyote wala siogopi kuwaita viongozi wa dini, kwa kuwa mmesimama mbele ya Wakristo na kuwatangazia habari njema kupitia nyimbo zenu.

Hivi sasa kuna jambo limezagaa na kuwachafua sana. Sitapenda kulizungumzia sana hilo, maana ni jambo ambalo bado linaonekana kuwa na makengeza lakini pia lipo kwenye mikono ya sheria.
Hata hivyo, sakata hilo linalomhusisha Emmanuel Mbasa na ubakaji halijafika mahakamani, hivyo bado linajadilika. Lakini sitafanya hivyo. Kuna mambo nataka kuwashauri kuhusu ndoa yenu.
Kinachonifanya niwaandikie barua ni namna sakata hilo lilivyo na hali ya ndoa yenu kwa sasa. Kwanza kabisa, inaonekana mlikuwa na mgogoro kwa muda mrefu hadi kufikia Flora kuondoka nyumbani na kwenda kuhamia hotelini!
Hapo Flora unawafundisha nini Wakristo? Kuna wimbo wako mmoja mzuri sana, unaitwa Maisha ya Ndoa, umeimba wewe na mumeo. Ni wimbo mzuri sana ambao unatia moyo wanandoa, vipi kwa upande wenu?
Ni kweli hapakuwa na namna nyingine ya mazungumzo hadi Flora ukaamua kuhamia hotelini badala ya kutatua lililoibuka katika ndoa yenu? Mke wa mtu utahamia vipi hotelini?
Nimesoma kwenye magazeti, Emmanuel anaonekana bado ana upendo na wewe, anakubali kuwa mna matatizo, lakini kwa nini Flora hutaki kumalizana na mumeo?

Flora dada yangu, nakushauri kwa kuwa wewe ni Mkristo unapaswa kuishi sawasawa na imani ya dini yako. Labda umeamua kuishi kwa taratibu za kimila, mbona pia hujazifuata?
Mke anapogombana na mume, kama anataka kufuata mambo ya kimila anapaswa kwenda nyumbani kwa mume. Ikishindikana zaidi anaweza kurudi nyumbani kwao. Kwa nini wewe umekwenda hotelini?
Mshenga yupo, wazee wa kanisa wapo, wachungaji wapo, kwa nini hotelini? Huoni unazidisha maswali kwa wadau wa Injili?

Hebu nirudi kwa Emmanuel, inawezekana tuhuma zinazomkabili ni za kweli, lakini watu wanaweza kujiuliza, kwa nini zimetokea wakati huu ambao Flora ameondoka nyumbani na kuhamia hotelini?
Maswali haya kibinadamu ni magumu mno kujibika, lakini kiroho ni mepesi hasa kwa ninyi mnaokula madhabahuni mwa Bwana. Angalieni, shetani anawajaribu na mnamruhusu!

Matokeo yake ni mabaya sana. Kama ni mchezo unafanyika na mnaujua ukweli, mjue kuwa Mungu anachukizwa na jambo hilo. Msingi wa ndoa ni kudumu hadi kifo kiwatenganishe.
Hakuna kuchokana, kuna kurekebishana. Narudia tena, mkataeni shetani anayewajaribu. Damu ya Yesu Kristo iwafunike na iwasimamie katika kipindi hiki chenye giza. Kwa Yesu hakuna kinachoshindana, Yuleyule, Mkweli daima, Joseph Shaluwa.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger