Tumekwisha! Mzee wa kanisa la kiroho (jina linahifadhiwa kwa sasa),
aliyetajwa kwa jina la Luca Pesa, mkazi wa Segerea, Dar, ameaibika baada
ya kukurupushwa kwenye nyumba ya kulala wageni (gesti) akidaiwa kutaka
kuvunja amri ya sita na binti ambaye ni msanii chipukizi wa filamu za
Kibongo, Debora Jacob, Ijumaa lina kisanga cha aina yake.
HABARI KAMILI
Tukio hilo ambalo kamwe Luca hawezi kulisahahu
maishani mwake, lilijiri kwenye gesti hiyo iliyopo karibu na Kituo Kikuu
cha Mabasi cha Segerea, Dar, Jumanne iliyopita huku mzee huyo
akishushiwa tuhuma nzito ya rushwa ya ngono kwa vibinti chini ya miaka
18.
Katika tukio hilo, mzee huyo wa kanisa na msanii huyo wa Kundi la
Maigizo la Vivif lenye maskani yake maeneo hayo walikuwa wamejichimbia
kwenye gesti hiyo katika chumba ambacho mlangoni kilikuwa kimeandikwa
Rombo kabla ya kuchomolewa na kufikishwa kanisani kisha polisi.
TUHUMA NZITO
Timu ya Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global
Publishers, ikiwa kwenye mingo zake, ilipokea simu kutoka kwa dada
aliyejitambulisha kwa jina moja la Diana na kujieleza kuwa anatoka kundi
la sanaa za maigizo la Vivif lililopo Segerea jijini Dar.
OFM: Ndiyo hujakosea unazungumza na
OFM, tukusaidie nini?
Diana: Kuna mzee wa kanisa la kiroho la (anataja jina la kanisa hilo)
lililopo maeneo ya Segerea, aliomba kuwa mfadhili wa kundi letu.
Tulimkubalia na baada ya muda alianza kutumia fedha zake vibaya kwa kufanya vitendo visivyofaa.
OFM: Vitendo gani visivyofaa?
Diana: Anawarubuni mabinti wadogo anawaweka kambini na kula nao tunda tamtam eti ndiyo tiketi ya kuchezeshwa kwenye maigizo.
OFM: Tiririka!
Diana: Yaani hadi muda huu ninapozungumza na ninyi mzee huyo wa
kanisa anachati na msanii mwingine wa kundi hilo. Anaitwa Debora anataka
waende kwenye gesti fulani wakanogeshane, wahini tayari mtego umewekwa
utafyatuka muda wowote.
UDHALILISHWAJI?
Diana alisema baada ya Debora kuombwa ‘mambo’
ndipo akawataarifu wasanii wenzake na kuwataka wote kwa pamoja waungane
kuikomesha tabia hiyo chafu ya Luca anayelichafua kanisa la kiroho na
kulidhalilisha kundi lao la sanaa.
OFM MZIGONI
Baada ya kuseti kila kitu, Diana aliiomba OFM
iambatane nao kwani muda huo tayari Debora alishatangulia kwenye gesti
hiyo kumfuata mzee huyo wa kanisa ambaye alishachukua chumba.
Taarifa hiyo ilipokelewa kwa mikono miwili na kiongozi wa OFM ambaye
aliwaagiza vijana wake makini ambao walisitisha kazi nyingine za
kiintelijensia kisha kuelekeza nguvu zao eneo la tukio.
Vijana hao
walitumia pikipiki zao ziendazo kasi ambapo baada ya muda usiozidi
dakika ishirini walikuwa wamefika kwenye gesti hiyo.
ENEO LA TUKIO
OFM walipofika eneo la tukio, walikuta kundi la
wasanii hao wakimchomoa gesti mzee huyo wa kanisa ambaye aliruka ukuta
na kudondokea kwenye matuta ya viazi.
Akiwa anajizoazoa kwenye matuta hayo, kundi la wasanii hao
lilimuunganishia ambapo kabla ya kumnasa aliingia kwenye chumba cha
nyumba iliyopo jirani na gesti hiyo ili kujisalimisha.
Hata hivyo,
zoezi lake lilifeli baada ya wasanii hao kumtahadhalisha mwenye nyumba
hiyo kuwa wanamtaka mtuhumiwa wao la sivyo wangeichoma moto.
Baada ya kuzingirwa na wasanii hao huku akihatarisha maisha yake kwa
kuwa wasanii hao walikuwa na hasira, aliona yasiwe makuu akaamua
kuwaruhusu wamtoe mtuhumiwa wao wakamalizane naye kanisani.
KABANG!
Alipotiwa mikononi, mzee huyo wa kanisa aliomba apelekwe
kanisani ambapo hapakuwa mbali na eneo la tukio ili akahifadhi vitu
vyake muhimu pamoja na kuomba ushauri.
APELEKWA MSOBEMSOBE KANISANI
Kundi hilo la wasanii lilimpeleka
kanisani msobemsobe ambapo baada ya hatua kadhaa polisi walitokea na
kuwadhibiti wananchi wenye hasira na wasanii waliotaka kumdhuru mzee
huyo wa kanisa wakati akipelekwa kanisani.
MTAANI WERAAA!
Wakiwa mitaani, njiani mabinti walikuwa wakipiga
kelele ‘weraaa…ukomeee…’ huku wakifurahia kufunga mitaa kwa madai kwamba
mzee huyo wa kanisa alizidi.
Katika sekeseke hilo, polisi hao walimtia pingu mzee huyo wa kanisa na kuongoza safari ya kuelekea kanisani.
Wakiwa kanisani hapo polisi walijitambulisha na kuwauliza wachungaji
pamoja na waumini wa kanisa hilo kama walimfahamu mzee huyo wa kanisa.
BREKI YA KWANZA POLISI
Kundi la wazee pamoja na vijana wa kanisa
hilo walikiri kuwa Luca ni mmoja wa wazee wa kanisa hilo ndipo polisi
hao wakamruhusu kuwakabidhi baadhi ya vitu vyake ikiwemo simu na fedha
kisha breki ya kwanza ikawa Kituo cha Polisi cha Tabata-Shule ambapo
alifunguliwa jalada la kesi namba RB/3843/2014 -RUSHWA YA NGONO,
KUWAWEKA KAMBI KINYUME CHA SHERIA WASICHANA WENYE UMRI CHINI YA MIAKA 18
NA KUWADHALILISHA KIJINSIA.
Hadi OFM wanaanua jamvi kituoni hapo kanisa lilikuwa likihaha kumchomoa kwa dhamana akisubiri sheria kuchukua mkondo wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment