Wakati hata siku arobaini hazijatimia, mke wa marehemu George Otieno
‘Tyson’, Beatrice Shayo juzi alicharukia mali zake baada ya kuamua
kutinga nyumbani kwa marehemu, Mbezi Makonde jijini Dar kwa lengo la
kuchukua kila kinachomhusu.
Mdada huyo aliyefunga ndoa na Tyson Agosti 9, 2012 nchini Kenya na
kujaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Eugene, alishuhudiwa na
gazeti hili Juni 24, mwaka huu saa sita usiku akiwa na ndugu zake na
kuanza kugonga geti la nyumba hiyo.
Katika kujua kilichokuwa kikiendelea, mmoja wa mapaparazi wetu
aliwasogelea na kuzungumza na Beatrice ambaye alieleza kuwa, lengo lake
lilikuwa ni kuchukua mali zake zilizomo mle ndani.
“Ulidhani mimi
nataka kuingia kwenye nyumba hii nikae, la hasha! Nimefuata mali zangu
tu basi,” alisema Beatrice huku akiendelea kugonga geti hilo.
Wakati Beatrice na nduguze wakionekana kukata tamaa ya kufunguliwa,
mara alitokea mwanamke anayedaiwa alikuwa akiishi na marehemu mpaka kifo
kilipomkuta na kuuliza aliyegonga geti ni nani, alipotajiwa jina la
Beatrice alisema: “Eee, Beatrice, usiku huu umekuja kutafuta nini?”
Beatrice: Nina shida, naomba ufungue tuongee.
Mwanamke: Hatuwezi kuongea usiku huu, uje kesho asubuhi.
Beatrice: Nakuomba ufungue tu, nimekuja kuchukua mali zangu nilizoacha humo ndani na nimekuja na gari kabisa la kubebea.
Mwanamke: Mali gani, humu hamna chako na kama una kitu chako humu, fuata taratibu.
Beatrice: Nimefuata taratibu, nipo na mjumbe hapa.
Mwanamke: Ndiyo nasema mje kesho asubuhi na mapema mtanikuta.
Baada ya mwanamke huyo kugoma kufungua, mjumbe wa eneo hilo
aliyefahamika kwa jina la Sabina Mawanda aliwashauri waondoke na kurudi
tena asubuhi lakini inadaiwa walipofanya hivyo walikuta nyumba imefungwa
na hakukuwa na mtu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment