Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa kabisa, ni siku
nyingine nzuri tunapokutana katika uwanja huu kujuzana mambo mbalimbali
yanayohusu uhusiano wa kimapenzi, hususan wachumba au wanandoa.
Kabla sijaanza kuijadili mada yetu ya hapo juu kama inavyojieleza, ningependa nikupe mfano mdogo kuhusu watoto mapacha.
Sote tunawajua watoto mapacha. Hawa huanza kuwa pamoja kuanzia wakiwa
kwenye tumbo la mama yao. Huzaliwa siku moja, hunyonya kwa pamoja na
hukua pamoja. Lakini siyo ajabu kuona watoto mapacha wakigombana hadi
kufikia hatua ya kuwekeana viapo au kutishia kuuana.
Sasa kama
watoto mapacha waliokaa pamoja tangu wakiwa tumboni mwa mama yao
wanagombana, ni dhahiri kwamba suala la ugomvi haliepukiki mahali popote
hasa katika uhusiano wa kimapenzi.
Kugombana, kukorofishana au kupishana kauli ni jambo la kawaida
kabisa kwa wapendanao na unapotokewa na jambo hilo, elewa kwamba
halijakupata wewe tu, hata Obama anagombana na mkewe Michelle wakiwa
ikulu itakuwa wewe?
Hata hivyo, kugombana ni jambo la kwanza lakini kuombana msamaha ni
jambo la pili. Haina maana kwamba kwa sababu kugombana hakuepukiki basi
kila unapogombana na umpendaye huo ndiyo uwe mwisho wa uhusiano wenu wa
kimapenzi. Hasira ni hisia za kibinadamu kama zilivyo hisia nyingine na
haziwezi kuepukika.
Jambo
la msingi ni kujiuliza, wewe unapokasirika huwa ‘unam-treat’ vipi
mpenzi wako? Huwa mnapata suluhu au muafaka baada ya muda gani? Moyo
wako huwa mwepesi kumsamehe mwenzako kwa urahisi au mpaka wiki au miezi
kadhaa ipite ndiyo umsamehe?
Je, unaweza kusamehe bure na kuyaacha maisha yaendelee au mpaka
ufanyiwe jambo kubwa kama kununuliwa zawadi za gharama ndiyo usamehe?
Bila shaka majibu utakuwa nayo mwenyewe.
Ninachotaka kuzungumza nawe
ni kwamba, hakuna jambo muhimu katika mapenzi kama kusamehe bila
masharti. Siyo tu kusamehe bali kusamehe katika muda muafaka.
Ikiwa mwenzako amekukosea leo na kukiri kisha akakuomba msamaha
lakini wewe kwa sababu ambazo unazijua mwenyewe, ukakataa msamaha wake
mpaka baada ya wiki mbili au mwezi kupita, msamaha wako utakuwa hauna
maana.
Hakuna mapenzi mahali ambapo hakuna msamaha. Unaposamehe haina maana
kwamba wewe ni dhaifu wala haina maana kwamba wewe ni mjinga. Tafsiri ya
mtu anayesamehe kwa urahisi ni kwamba anajitambua, anajiamini na
anaelewa kwamba hakuna binadamu aliyekamilika. Mapenzi bila kusameheana
kwa dhati, huyeyuka kama barafu iyeyukavyo juani.
Mwenzako anapokukosea, lazima jambo la kwanza ukumbuke kwamba hakuna
binadamu aliyekamilika. Kila mmoja ana mapungufu na mazuri yake. Badala
ya kutazama yale mabaya ambayo mwenzako amekufanyia, hebu jaribu
kutazama yale mazuri ambayo amekuwa akikutendea kila siku.
Ukifanya hivyo, utaona umuhimu wa kumsamehe haraka bila kumuacha ateseke kwa muda mrefu akiutafuta msamaha wako.
Acha tabia ya kutaka fidia kama njia ya kumsamehe umpendaye, wewe
msamehe bure halafu yeye kwa kuuheshimu msamaha wako, bila shaka
atakufanyia jambo zuri kama kukupa zawadi, kukutoa out au jambo lolote
zuri ambalo litakufurahisha.
Hata asipofanya hivyo, atakuheshimu ndani ya moyo wake na ataendelea
kukupenda. Ukimuacha alie, apige magoti, aumie moyo au afanye jambo
kubwa ndipo umsamehe, baadaye ataelewa kwamba kumbe huna huruma naye na
kwamba hujamsamehe kwa sababu unampenda ila ni kwa sababu amekufanyia
jambo fulani, kitu kinachoweza kufanya penzi lenu liendelee kufifia
kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.
Ni matumaini yangu kwa haya machache, tutakuwa tumeelewana vizuri.
Kumbuka penzi la kweli husamehe haraka na huwa na huruma. Hebu jifunze
kusamehe haraka na kuwa na huruma na mwenzako. Na wewe unayesamehewa,
usiwe mtu wa kukosea kila siku, jirekebishe ili mtimize ndoto zenu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment