UKWELI KAMILI WA FLORA MBASHA

MIMI ni mkristo wa dhehebu la Roma. Mafundisho mengi tunayopewa kuanzia Ubatizo, Komunyo ya Kwanza na Kipaimara, tunafundishwa kuhusu kutenda mema, kupendana wenyewe kwa wenyewe na hata kuwapenda maadui zetu.
Tunaambiwa, akija mtu akakupiga kofi shavu lako la  kushoto, wala hata usimrudishie, bali mgeuzie na upande ule wa kulia na akishakutundika hivyo vibao vyake, muombe Mwenyezi Mungu amsamehe. Tunafundishwa kusamehe, ndiyo maana katika moja ya maandiko yaliyo katika vitabu vya dini, kama Injili na Biblia, kuna mistari inayosema samehe saba mara sabini. 
Kwa wale ndugu zangu wasio wakristo, nitaomba niwaombe radhi kwa kuanza na utangulizi huu. Ni kwa sababu leo nazungumza na mtu ambaye wengi wetu tunaamini ni mtumishi wa Mungu. Mtu yeyote anayesambaza neno la Mungu, huwa ni mtumishi wake. Neno zuri la Mungu husambazwa kupitia mihadhara, misa, maombi na hata nyimbo kama Flora Mbasha anavyofanya. 
Leo nikiambiwa niwataje waimbaji wa Injili kumi bora nchini, jina la Flora Mbasha litakuwa katikati yao, likigawa kundi moja juu yake na lingine chini yake. Hii ni kwa sababu ni mmoja wa waimbaji wazuri wa muziki huu. Hujisikia furaha ninaposikiliza ujumbe uliomo katika nyimbo zao, ingawa baadhi ya kazi zake huchezeka, lakini ujumbe wake maridhawa hubakia kuwa fumbo. 
Familia ya watu wa muziki wa Injili nchini, imepata mshtuko mkubwa wiki chache zilizopita, baada ya waimbaji, ambao ni wanandoa, Emmanuel na Flora Mbasha kupamba vichwa vya habari baada ya kutokea mzozo wa kifamilia kati yao, ambao unadaiwa kusababisha mwanaume kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za ubakaji. 
Sitaki kuzungumzia suala lililopo kortini kwa sababu sheria zinakataza, isipokuwa nataka kuzungumza na mdogo wangu Flora kwa sababu alichokifanya katika kipindi chote cha mtafaruku baina yao, hakikupaswa kufanywa naye hasa kwa jinsi alivyofanikiwa kujitengenezea taswira ya kuheshimika mbele ya jamii. 
Huwa najaribu kusema mara nyingi, ustaa ambao baadhi yetu hatulali kwa kuutafuta una gharama kubwa. Ukishakuwa mtu maarufu, unajinyima baadhi ya haki zako za msingi, kama vile masuala yako binafsi kubaki kuwa ya kwako. 
Ninafahamu Flora, kama mke ana haki ya kukataa baadhi ya mambo kufanyika katika ndoa yake. Sisi tulio katika ndoa tunafahamu, kuna maisha magumu kweli, wakati mwingine mume na mke huweza kukaa hata mwezi mzima bila kuzungumza, lakini kwa sababu ya kuhifadhi matatizo yenu yasitoke nje, mnakaa kimya.  
Akija jirani, hawezi kujua kama hamzungumzi kwa namna mtakavyompokea kwa bashasha na kumpa ushirikiano. 
Kama kukaa kimya ili mambo hayo yaishe yenyewe kimyakimya mnashindwa, kinachotokea ni kuwafuata ndugu wa karibu, ambao mara nyingi huwa ni wale waliowazidi umri. Mnapeleka tatizo lenu, mnaitwa, mnajadiliana kwa pamoja, mnaondoka na muafaka! 
Haya mambo yangeweza kufanywa na Flora, hasa kwa kuwa jamii inamtambua kama mtu mwenye woga na Mungu. Sasa kama mtu anayetakiwa kuwa mfano, anaondoka nyumbani kwake na kwenda kusikojulikana, tena wakati mumewe akiwa katika matatizo, unataka watu wakutazame kwa macho yapi?  
 
itaki kusema nani mwenye makosa kati yao, ninachotaka kusema ni kitendo cha Flora kuifanya jamii ione ni kama anayefurahia matatizo yanayomzonga mumewe. Hii siyo sawa, hata kama ndani hatuongei, nje sisi ni kitu kimoja. 
Wakati akiwa madarakani, Rais wa Marekani, Bill Clinton aliwahi kukutwa na tuhuma za kumbaka mfanyakazi wa Ikulu, Monica Lewinsky. Katika kipindi chote cha sakata hilo, mkewe Hilary, alikuwa upande wake, hakumuacha, alikuwa tayari kufa naye, kuliko kuongeza petrol kwenye moto. Nani anajua waliishije wakiwa chumbani kwao? 
Flora anatakiwa kutambua kuwa kuna ndoa chache sana zinaishi kwa upendo kama tunavyoziona. Kitu kikubwa tunachopaswa kufanya, hasa kwa mastaa ni kuzilinda ndoa zetu kwa mikono yetu wenyewe.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger