Habari hiyo ilimhusu mtoto Salum Kassim wa miaka 16 anayesumbuliwa na
tatizo la tumbo kujaa maji na kulifanya kuwa kubwa sana huku madaktari
wakisema chanzo ni hitilafu kwenye moyo.
Baada ya maelezo ya mtoto huyo kuhusu ugonjwa huo mbaya na maisha
duni anayoishi, ilionekana kuwa mlezi wake amekuwa akitumia shilingi
elfu kumi (10, 000) kila mwezi kununua dawa za kutuliza maumivu
anayoyapata na si kumaliza tatizo.
Hata hivyo, kuna mwezi mtoto huyo anapitiliza bila kupata dawa baada
ya mlezi wake kutokuwa na kiasi hicho cha pesa hali inayomsababishia
kupoteza mpangilio wa dozi.
Mwisho wa habari tuliandika namba za
simu za mlezi wa mtoto huyo kwenda kwa Watanzania watakaoguswa na afya
tete ya Salum kumchangia ili aweze kupata tiba sahihi na hivyo kuokoa
uhai wake ambao upo hatarini kwa mujibu wa madaktari.
Sasa kwa mujibu wa mlezi wa mtoto huyo, tangu gazeti hilo kutoka
mpaka juzi, Julai 8, mwaka huu wasamaria wema wamejitokeza kumsaidia
mtoto huyo ambapo kiasi cha shilingi 300,000 zimeshachangwa huku wengine
wakiahidi. Hii ni dalili njema!
Aidha, Julai 2, mwaka huu, waandishi wa Global walikwenda Hospitali
ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa lengo la kuangalia
uwezekano wa kumpeleka mtoto Salum kuanza vipimo lakini daktari mmoja
alisema atatoa jibu lini apelekwe bila kufafanua sababu za kusema hivyo
licha ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa ufunguzi wa taasisi hiyo kutoa
maelekezo kwamba, iwasaidie Watanzania, hasa walalahoi, bila kuweka
vikwazo.
Mlezi wa mtoto huyo amesema kuwa, licha ya maradhi yanayomsumbua
Salum, anakabiliwa na changamoto zingine zinazohitaji kutatuliwa kwa
fedha kama chakula, sabuni, mafuta ya kupaka mwilini, maji ya kunywa,
dawa ya meno pamoja na mavazi.
Ili kumsaidia mtoto Salum, endelea na moyo wa kutoa kwa kutuma kiasi
chochote cha pesa kwenda namba 0785 999 276 na 0682 865248. Namba zote
ni za mlezi wa mtoto huyo. Magazeti ya Global yataendelea kutoa
maendeleo yake kila wakati.
Ndugu msomaji, kumbuka kutoa ni moyo hivyo msaidie mtoto huyu upate baraka. Mhariri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment