MASIKITIKO: MAITI YA MBONGO YAWEKWA MOCHWARI CHINA MIEZI 8


VILIO, majonzi vilitawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Agosti 7, mwaka huu kufuatia kuwasili kwa mwili wa mwanafunzi wa kidato cha nne, Habiba Yusuph Ally (24) aliyefariki dunia kwa kubakwa nchini China miezi nane iliyopita.
Mwili wa Habiba Yusuph Ally (24) ukiwa katika jeneza eneo la uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Tukio hilo linaweka historia ya kusikitisha kwenye familia ya mzee Yusuph Ally kwa kuwa na msiba miezi nane wakati mwili wa binti yake ukiwa mochwari nchini humo baada ya kifo chake.
Habiba Yusuph Ally enzi za uhai wake.
KWA NINI MIEZI NANE?
Akizungumza na Uwazi kwa masikitiko makubwa, baba wa marehemu alisema kilichosababisha maiti ya binti yake ikae mochwari kwa muda wote huo ni utafutaji wa fedha kuwa mgumu lakini hatimaye Watanzania waishio nchini humo walifanikisha na kuuleta kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.

Mwili wa Habiba Yusuph Ally ukichukuliwa kutoka uwanja wa ndege.
ALICHOKIONA BABA CHAMSHTUA
Mara baada ya mwili huo kuwasili, kilifika kipengele cha kufunuliwa ili baba mzazi amtambue marehemu ambapo zoezi hilo lilimshtua mzee huyo kufuatia kuuona uso wa mwanaye ukiwa na majeraha kibao huku tumbo likiwa limeshonwa. Ilidaiwa ulifanyiwa uchunguzi.

MWILI WAPELEKWA NYUMBANI
Baada ya hapo, mwili huo ulipekekwa nyumbani kwa mzee Yusuph kwa ajili ya kuagwa na siku iliyofuata, Agosti 8, mwaka huu ukazikwa kwenye Makaburi ya Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam.

Mwili wa marehemu, Habiba Yusuph Ally ukipakiwa kwenye gari .
HABIBA ALIVYOKUFA
Katika gazeti ndugu na hili, Ijumaa Wikienda Toleo la Februari 24, mwaka huu liliandika habari ya kubakwa kwa Habiba hadi kufariki dunia. Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka; MBONGO ABAKWA CHINA, AFA! Kwa mujibu wa baba, Habiba alibakwa Januari 18, mwaka huu.

Maelezo ya habari hiyo yaliyotolewa na rafiki wa karibu wa Habiba aitwaye Saada yalisema siku ya tukio, marehemu alikutana na Mnigeria mmoja ambaye walipatana kulala wote kwa usiku mzima.
Alisema kumbe Mnaigeria huyo alikuwa na wenzake wanne. Usiku walimwingilia wote kwa nguvu mpaka akapoteza maisha palepale. Ulikuwa ukatili mkubwa.

Watu hao walipogundua Habiba amefariki dunia  waliuchukua mwili wake na kuutupa chini kutoka ghorofa ya tano walikokuwa wamempeleka kulala naye.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa msibani.
Habari zaidi zilidai kuwa madaktari waliokuwa wakiuchunguza mwili wa Habiba waligundua haukuwa na figo na moyo jambo lililozidi kuzua hofu juu ya mauaji yake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mzee Yusuph juzi, Wanigeria hao walikamatwa na jeshi la polisi nchini humo na kufikishwa mahakamani kwa kudaiwa kuua.

Alisema mara baada ya kifo, polisi nchini humo waliizua maiti yake kwa muda ili kupisha upelelezi zaidi na baada ya kukamilika ndipo Watanzania walioko huko wakaanzisha mchango wa fedha kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania, China na kuusafirisha mwili wake.
MBONGO AONGEA
Uwazi lilibahatika kuzungumza kwa simu na Mtanzania anayeishi kwenye Mji wa Guangzhou nchini China (jina tunalo) ambaye alidai nguvu kubwa ilitumika kuchangishana fedha ili kuuleta Bongo mwili wa marehemu Habiba.

Masheikh wakiuswalia mwili wa Habiba kwa safari yake ya mwisho.
ATOA USHAURI
Mbongo huyo anayefanya biashara nchini humo alitoa ushauri kwa Watanzania wenye ndugu China kuwa makini nao kwa vile wengi wakifa, kama hakuna moyo wa kuchangiana huzikwa na taasisi zinazosimamia kazi hizo lakini ikibainika kuwa kuna michango inayoendelea, mwili unaweza kuwekwa mochwari hata miaka miwili.

HISTORIA YA MAREHEMU HABIBA
Marehemu Habiba aliondoka Bongo kwenda China mwaka 2010 akiwa na miaka 19 akisoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kiluvya, Kinondoni, Dar kufuatia kurubuniwa na mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Chausiku.

Vijana wakiushusha mwili wa Habiba kaburini.
Kwa mujibu wa baba wa marehemu, marehemu Habiba alikuwa mtoto wa tano kati ya saba, aliondoka nchini na mwanamke huyo bila kumwambia ndugu yeyote.
“Alirubuniwa na huyo Chausiku kwamba anakwenda kufanya kazi saluni lakini alipofika kule akamwingiza mwanangu kwenye biashara ya ukahaba. Hata hao waliombaka walimpata kwenye biashara hiyo,” alisema baba wa marehemu.
Wakati wa Mazishi ya Habiba.
Akaongeza: “Sisi tukiwa hatujui alipo, miezi minne ilipita akampigia simu mama yake na kumwambia yupo Dubai anafanya kazi, tulipochunguza namba ilionesha yupo China, tukaambiwa huwa hawatakiwi kusema ukweli wa sehemu walipo.”
BIASHARA ILIVYO
Uchunguzi unaonesha kuwa, mawakala wanaosafirisha wasichana wa Kibongo kwenda China, Dubai au India, wakifika, huwanyang’anya hati zao za kusafiria ili washindwe kuondoka nchini humo na kushinikizwa kujiuza (ukahaba) huku wao mawakala wakipokea fedha kutoka kwa wateja.

Uchunguzi unaonesha wasichana hao hurejeshewa hati zao baada ya malipo ya kiasi cha Dola za Marekani 8,000 (kama shilingi milioni 12).
Marehemu Habiba Yusuph Ally (kushoto) wakati akiwa shule.
Wengi wakishaachiwa hushindwa kurejea Bongo na kujikuta wakiendelea kuuza miili katika mahoteli na klabu huku wakikutana na majanga mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger