DUNIANI kuna mengi kiasi kwamba kama mama
umebeba ujauzito kwa miezi tisa na kujifungua mtoto salama na mtoto wako
ni mzima unapaswa kumshukuru Mungu kwani kuna watu ambao wanapata
usingizi wa mang’amung’amu kutokana na mateso ya watoto wao.
Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3), mkazi wa Kijiji cha Kamala, Kata
ya Bangwe mkoani Kigoma yupo ndani ya mateso makubwa yanayomfanya kulia
muda wote kutokana na maumivu makali anayoyapata kwa ugonjwa wa kansa
unaotafuna macho yake hivyo kumfanya asione.
HISTORIA YAKE
Akizungumza na Uwazi akiwa katika masikitiko makubwa
nyumbani kwa ndugu yake, Manzese jijini Dar, bibi wa mtoto huyo
aliyejitambulisha kwa jina la Elda Charles Rweyemamu, mjukuu wake huyo
alizaliwa akiwa hana tatizo lolote lakini alipofikisha umri wa miaka
miwili na nusu akapatwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho upande wa kushoto.
“Tuliamua kumpeleka kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni ambapo
alitibwa akapata nafuu, tukarudi nyumbani.“Lakini wanasema ukizaliwa na
balaa ni balaa tu, mwanzo hadi mwisho.
Kwani baada ya muda ugonjwa ulijirudia tena, sasa si mtoto wa jicho
ila jicho likaonekana kuwa na uvimbe kidogo. Mimi na mama yake
tulishangaa sana, tukaona lazima tuendelee kuhangaika. Tukampeleka
katika Hospitali ya Matiazo.
“Madaktari walijitahidi, wakamtibu akapata nafuu tena na uvimbe katika jicho uliisha, tukajua tumeepukana na hilo.
UGONJWA WARUDI KWA KASI
Akiendeleza kusimulia mateso ya mtoto huyo, bibi huyo alisema:
“Baada ya kukaa kwa muda mfupi, ghafla ugonjwa ulirudi tena, sasa eti
hata kichwa kilivimba. Hii hali ilitushangaza sana na tukawa tunaulizana
ni nini?
“Nilimwambia mama yake kuwa Mungu ni wa kumtumaini muda wote, hivyo
tukampeleka tena Hospitali ya Maweni lakini madaktari wakasema ili
mjukuu wangu aendelee kuwa na uhai tuje hapa Muhimbili. Tulifunga safari
ya kuja ambapo Julai 21, mwaka huu, tukawa tumefika.”
MATUMAINI YAREJEA, YAYEYUKA
“Tulipofika hapa
Muhimbili na kuona hospitali yenyewe ilivyo kubwa na madaktari bingwa
wengi niliamini kuwa mjukuu wangu angepona na kurudi naye nyumbani akiwa
salama lakini cha kushangaza mambo yakawa tofauti na jinsi nilivyokuwa
nikifikiria.
”Madaktari walimfanyia uchunguzi, baada ya siku nne waliniambia ugonjwa alio nao huyu mtoto ni kansa.
“Walinitoa machozi zaidi pale waliponiambia kuwa, hata hivyo hawataweza kumtibu kwa vile tulichelewa kumleta.”
“Lakini hata wao waliniambia wakiwa na masikitiko makubwa kwani
nilishangaa kuwaona baadhi ya madaktari wakitoa machozi kwa kumuonea
huruma mjukuu wangu kwa jinsi anavyolia muda wote kwa maumivu kama
unavyomsikia,” alisema.
Aliongeza kuwa, walichofanya madaktari hao ni kumpa dawa ya kutuliza
maumivu na kumwambia bibi mtu warudi nyumbani Kigoma kwa ajili ya
kumshukuru Mungu kwa yote.
HANA NAMNA YA KURUDI KIGOMA
“Tangu nimeruhusiwa
kutoka Muhimbili, Julai 26, mwaka huu sina jinsi ya kurudi nyumbani
Kigoma. Nauli hadi kule ni shilingi 70,000. Kwa sasa nimepata hifadhi
hapa Manzese kwa mdogo wangu ambaye anaishi kwa kufanya biashara
ndogondogo lakini hana fedha. Kuendelea kukaa kwake ni sawa na kero
kwani huyu mtoto amekuwa akilia mara kwa mara hali ambayo ni kero kwa
wapangaji wenzake.
“Hata chakula ni tatizo, kila siku inabidi nimpeleke katika zahanati
kusafisha macho. Kwa muda wa wiki moja nimetumia shilingi 300,000 kwani
aliishiwa damu na inabidi aongezwe halafu kuna dawa za kutuliza maumivu
aliongezewa, nina shida kubwa sana.”
KWA NINI BIBI NA MJUKUU?
“Kilichonifanya nije
mimi huku Dar ni kwa vile mama yake ni mjamzito. Wakati wowote anaweza
akajifungua. Pia ana mawazo mengi sana kwani watoto wake wawili, wa
kwanza na wa pili walifariki dunia kutokana na magonjwa ya aina
mbalimbali na huyu wa tatu ndiyo madaktari wamesema nimrudishe nyumbani
tusuburi kifo,” alisema Elda kwa huzuniu
ANACHOOMBA
Anachoomba bibi huyo ni nauli ya kumuwezesha kurudi nyumbani kwake, Kigoma. Kwa aliyetayari anaweza kumsaidia kupitia namba 0762 175 117, 0784 420 215 au 0719 285 100.
Ndugu msomaji, kama ulivyosikia kilio cha bibi huyo ambaye yupo
katika wakati mgumu wa kumuuguza mjukuu wake, hebu msaidie kwa chochote
ulichonacho, tunaamini Mwenyezi Mungu atakubariki. Mhariri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment