BAADA YA KUTOKA JELA , BABU SEYA NA PAPII KOCHA WATAFUTA STAIL MPYA YA KURUDI NAYO URAIANI



  Babu Seya na Papii Kocha wakiwa nje ya mahakama.

MAISHA ya uraiani baada ya kutoka gerezani ndiyo mzozo uliopo sasa kati ya wanamuziki mahiri nchini ambao ni baba na mwana, Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, Amani limetonywa. 


Chanzo makini kimesema kuwa wawili hao wamefikia hali hiyo baada ya kila mmoja kuanika dira ya maisha yake ya uraiani baada ya kuachiwa kutoka katika kutumikia kifungo cha maisha jela katika Gereza la Ukonga.

MAISHA YAO YANAPISHANA
Kwa mujibu wa chanzo, inadaiwa kuwa Papii Kocha aliulizwa na baba yake maisha yake ya uraiani yatakuwa ya aina gani ambapo bila kupepesa macho alisema atarudia kazi ya muziki kama zamani.



“Ishu kubwa ni maisha ya uraiani, Papii amemhakikishia baba yake kwamba akiwa uraiani ataendelea na muziki jambo ambalo Babu Seya hakubaliani nalo hata kidogo,” kilisema chanzo cha ndani. 



Kikaendelea: “Unajua yule mzee (Babu Seya) yeye anaamini kwamba uraiani lazima wabadili staili ya maisha kwa vile kuwa kwao huru kuna mkono wa Mungu kwa hiyo kuendelea kuishi maisha ya kidunia ni kutorudisha shukurani kwake.”


 
Nguza Viking ‘Babu Seya’ (wa pili kulia) na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ (wa pili kushoto) wakiwa mahakamani.

MSIMAMO WA BABU SEYA 
Wakati Papii Kocha akianika msimamo huo kwa baba yake ambao ulisababisha wazozane, mzee huyo yeye ameweka wazi kwamba maisha yake ya uraiani ni ya kumtumikia Mungu mwanzo mwisho.



“Lakini Babu Seya alimlaumu sana mwanaye kwamba kuendelea kufanya mambo ya duniani ni kutomtendea haki Mungu kwa vile nguvu zake ndiyo mwanga wa maisha yao mapya,” kilisema chanzo. 



HAYA YOTE YAMEKUJAJE?
Chanzo kilisema mambo hayo yote yameibuka kufuatia rufaa zote za wafungwa hao kupigwa chini na hivyo hatima yao kuwa mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’ ambapo wanaamini wapo huru tayari kinachosubiriwa ni siku tu.



Chanzo: “Unajua imani ni kitu cha ajabu sana. Yeye (Babu Seya) anachoamini wapo huru tayari, ila siku ndiyo ya kuvutia subira lakini pia anaamini mbali na msamaha wa JK, Mungu anatenda.” 


BABU SEYA ATATUA KANISA LA LIFE IN CHRIST
Dodosa zaidi za ndani zinaweka wazi kwamba, msimamo wa Babu Seya kwa maisha ya uraiani ni kuabudu kwenye Kanisa la Life in Christ Ministries (Zoe) lililopo Tabata Segerea jijini Dar ambako ndiko anakotoa huduma mtoto wake aliyeachiwa huru katika kesi hiyo na Mahakama ya Rufaa Tanzania, Nguza Mbangu.





 
Babu Seya na Papii Kocha wakiwa nje ya mahakama.

NGUZA MBANGU AONGEA NA AMANI
Baada ya taarifa zote hizo, juzi Amani lilimtafuta Nguza Mbangu ili kumsikia alichonacho kuhusu maisha ya baba yake uraiani, hasa suala la kuokoka na kumrudia Mungu.



Mbangu: “Suala la kuokoka ni la Mungu mwenyewe akiamua kumvuta mtu. Kama nia ya moyo wake ni hiyo basi ina maana mzee (baba) ameshavutwa. 



“Kwanza nataka nikwambie kitu Ndauka, siku zile baba na Papii waliposhindwa rufaa magazeti yaliandika sana, ooooh! Babu Seya na mwanaye kufia jela. Mimi nakwambia hivi, suala la baba na Johnson (Papii) watu wamekuwa wakiliangalia kimwili. 



“Mimi ninachojua wale wapo huru hata leo hii (juzi Jumanne), nilishakwambia siku za nyuma na leo narudia tena, Tanzania itamshangaa sana Mungu kupitia wale watu (Babu Seya na Papii).



“Tena nakuahidi kwamba, siku si nyingi, pengine mwezi huuhuu. Yaani, sijui nikwambiaje, nitakupigia simu, nadhani keshokutwa (leo Alhamisi), ndipo utajua nilikuwa namaanisha nini,” alisema Mbangu kwa kujiamini. 



TUREJEE NYUMA 
Juni 25, 2004, Babu Seya, Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza walihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji na kuwanajisi watoto 8 wa Shule ya Msingi, Mashujaa, Sinza jijini Dar. Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu chini ya Hakimu Eddy Lyamuya. Walikata rufaa Mahakama Kuu. 



Januari 27, 2005 rufaa yao ya kwanza ilisikilizwa ambapo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo aliitupilia mbali. 


Februari 10, 2010 Mahakama ya Rufaa ilikazia hukumu ya Kisutu kwa Babu Seya na Papii Kocha, lakini ikawaachia huru watoto wengine wawili wa mwanamuziki huyo, Nguza Mbangu na Francis Nguza
 

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger