Kwako Kajala Masanja. Bila shaka ni mzima wa afya. Binafsi mimi niko poa na ninaendelea na majukumu yangu kama kawaida.
Leo nimekukumbuka kupitia safu hii, nataka kuzungumza na wewe, na
hasa katika suala zima la ‘ku-maintain’ ustaa wako.Ninaposema ustaa
wako, namaanisha heshima, kipaji (kazi) pamoja na mapato yako.
Juzi kupitia gazeti la Ijumaa Wikienda tumeona jinsi gani umepiga
hatua kimaisha. Umetoka katika maisha ya kuonekana wa kawaida, sasa
unapewa heshima ambayo sidhani kama uliwahi kuitegemea kama unaweza
kuipata.
Ulikuwa mtu wa karibu na aliyekuwa shosti wako, Wema Sepetu ‘Madam’
ambaye wakati huo alikuwa ana mkwanja mrefu kuliko wewe, jinsi fedha
ilivyo mwana haramu kwa wakati huo ilikuwa ikiwezekana kabisa Wema
akakutuma kitu, ukatii.
Jeuri ya fedha aliyoionesha Wema wakati wa matatizo yako alipokutolea
shilingi milioni 13, inaonesha ni jinsi gani mwenzako alikuwa vizuri
kifedha. Akakuokoa kwenye kifungo na wewe ukarudi uraiani.Unakumbuka
vizuri hata baada ya yeye kukutolea fedha hizo nini kiliendelea katika
maisha yenu, starehe mwanzo mwisho.
Mlikuwa mkiongozana na timu ya watu katika kumbi mbalimbali za
starehe mkionesha jeuri ya fedha. Najua unakumbuka Wema alivyofanya
mbwembwe na fedha nyingi kumleta msanii wa Nigeria, Omotola Jalade
Ekeinde kuja kuzindua filamu yake ya Super Star ambayo haijaingia sokoni
hadi leo.
Kwa jeuri hiyo na nyingine nyingi alizokuwa akizifanya Madam, hakuna
ambaye aliwaza kwamba siku moja ufujaji wa fedha unaweza kubadilika na
kuwa fedha za mawazo.Hakuna aliyewaza kwamba wewe ambaye ulikuwa chini
yake ungeweza kuja kuwa juu yake.
Hakuna linaloshindikana chini ya jua na sasa kibao kimegeuka, sasa
fedha imekutembelea.Heshima ile ambayo alikuwa akiipata aliyekuwa shosti
wako, unaipata wewe.Hapo ndipo unapotakiwa kupatazama kwa makini.
Kama umefanikiwa kufungua kampuni yako ya kuzalisha filamu, iwekee
misingi thabiti isije kuyeyuka kama ilivyoyeyuka ya huyo aliyekuwa
shosti wako (Wema).Tengeneza mazingira ya kuzalisha kazi na kuziuza
kweli Watanzania waone kwamba kuna filamu bora zinazalishwa kutoka
katika kampuni yako.
Kuwa na fedha nyingi na kutokokuwa na mipango mipya ya kuzizalisha,
ni rahisi kupotea na kurudi kule ulikotoka.Njia aliyopitia aliyekuwa
shosti wako iwe funzo kwako. Chagua njia sahihi ili uendelee kuwa makini
katika maisha yako.
Asikwambie mtu, starehe za kupindukia huku ukiamini ‘bado zipo benki’
ndiyo chanzo cha wengi kuporomoka.Natumai sijachelewa kuzungumza na
wewe maneno haya machache, yafanyie kazi ili usije kujifunika shuka
wakati kumekucha. Mungu akubariki!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment