Ni hali ya kusikitisha na kustaajabu kwa jamii baada ya Tunu Kimaro
kummwagia maji ya moto mumewe, William Mushi (32), mkazi wa Mabibo
jijini Dar es Salaam pamoja na mtoto wake mchanga. Tukio hilo la
kikatili lilitokea Agosti 15, mwaka huu nyumbani kwake Mabibo jijini Dar
es Salaam na lilishangaza majirani kutokana na Tunu kudaiwa kuchukuwa
maji ya moto yaliyokuwa yanachemka na kuwamwagia bila huruma.
CHANZO NI MTOTO
Akisumulia mkasa huo Mushi alikuwa na haya ya kusema:
“Mke wangu anaitwa Tunu Kimaro ana miaka 23. Alinimwagia maji ya moto
baada ya kumkuta mwanangu wa miezi saba hali yake ya kiafya ikiwa siyo
nzuri, nilipokuwa naondoka asubuhi nilimuagiza ampeleke hospitali.
“Baada ya kufika nyumbani na kumkuta mwanagu Ivan amenyong’onyea,
nilipomuuliza mke wangu sababu za kutompeleka hospitali alinijibu majibu
ya kijeuri kama siyo mke wangu na mtoto siyo wake.
“Niliendelea kumtaka anieleze sababu ya kutompeleka mtoto wetu hospitali ndipo aliposema ngoja anioneshe.
“Alitoka nje kumbe alikuwa anachemsha maji, alikuja nayo yakiwa
kwenye sufuria aliloshika kwa kitambaa, akatumwagia mimi na mwanangu
ambaye anajua hajui chochote,” alisema Mushi.
LENGO LAKE KUTUUA
Akaongeza: “Naamini lengo lake
lilikuwa ni kutuua na si vinginevyo. Ni jambo la kusikitisha sana na
majirani nao walisoneneshwa na tukio hili baya.
“Ni vyema angesubiri niwe peke yangu, lakini alitumwagia maji akijua
kuwa nina mtoto tena mchanga. Nashukuru Mungu kwa sababu nilijitahidi
kumkwepesha na maji yale ya moto, lakini yalimpata na kumuunguza kama
unavyoona.”
AKIMBILIA POLISI
Mume huyo alisema: “Baada ya mke wangu kutufanyia kitendo kile alikimbilia polisi na kudai eti kuna mtu amemshambulia.
“lakini baadaye nilipopelekwa polisi kuchukua PF 3 (hati ya kuruhusu
nitibiwe), askari walishangaa kuona nilivyounguzwa mimi na mwanangu na
walipigwa na butwaa nilipowaeleza kuwa aliyefanya hivyo ni mke wangu.
“Askari polisi baada ya kupata ukweli ilibidi mke wangu awekwe ndani
ili aweze kutoa maelelezo ilikuwaje. Nashindwa kuelewa kama sababu ni
kumlaumu kwa kutompeleka hosptali mtoto wetu au kuna jambo lingine.
“Nahisi kuna mtu anamtia kiburi kwa sababu mke wangu hakuwa na tabia
hizi za kujibu kijeuri na moyo wa kikatili, watu wengine walidhani huyu
mtoto yupo kwa mama wa kambo,” alisema Mushi.
Majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mtoto amelazwa katika kitengo cha watoto walioungua.
AFISA WA POLISI ANENA
Mama wa mtoto huyo
anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Urafiki, jijini Dar es Salaam
ambapo afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwa
kuwa siyo msemaji alisema upelelezi ukikamilika ni lazima sheria ichukue
mkondo wake.
MUUGUZI ANASEMAJE?
Muuguzi aliyekuwa zamu siku
hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Cristene Chilambo, alishangazwa na
kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo na kuongeza kuwa hali ya mtoto
inaendelea vizuri.
“Mtoto huyu hana kosa lolote, mama yake amekosea
sana na naomba taasisi za haki za binadamu zifanyie kazi ukatili huu
maana huu ni unyama na ukatili wa aina yake,” alisema Chilambo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment