
Mmkazi wa Ludewa, Mkoani Njombe, Yohana Nkwera (54) anadai kukatika miguu katika hali ya kushangaza.
Yohana anasema katika maisha yake
amekuwa ni mwenye hofu kubwa baada ya kukumbwa na tukio hilo la aina
yake la kukatika miguu akiwa usingizini. Anasema hadi sasa haelewi namna
hasa tukio hilo lilivyomtokea, kwani hakuhisi maumivu yoyote .
Anasema tukio hilo la aina yake
lilimtokea mwaka 1992, lakini halikuwahi kuandikwa wala kutangazwa,
badala yake ni watu wachache waliokuwa wakilifahamu.
Anasema siku hiyo usiku alikwenda kulala kama ilivyo kawaida, alipoamka asubuhi alikuta miguu yake imekatika.
Kilichomshangaza zaidi ni kwamba
hapakuwa na damu wala jeraha lilionekana. Palionekana pana kovu, kana
kwamba alikatika mguu muda mrefu uliopita.
Anasema mara ya kwanza ulianza kupotea
mguu wa kulia, hiyo ilikuwa ni mwezi Machi, 1992. Kutokana na tukio
hilo, ndugu zangu walifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya maombi
katika nyumba mbalimbali za ibada, huku wengine wakienda kwa kuwaona
waganga wa jadi.
“Kama binadamu wa kawaida ilichukua muda sana kuamini kilichotokea ndani ya maisha yangu na mguu wangu,” anasema.
Mwezi mmoja baadaye yaani mwezi Aprili
mguu wa kushoto nao ulikatika katika mazingira yaliyo sawa na yale ya
awali.Inaweza kuwa vigumu kuamini lakini ulimwengu ndivyo ulivyo.
Anakumbuka mazingira ya kukatika kwake
yanahusishwa na imani za kishirikina kwa sababu siku chache zilizopita
kabla ya kukumbana na dhahama hiyo aliwahi kukorofisha na mtu katika
vilabu vya pombe za kienyeji anayesadikiwa kufanya tendo hilo.
Baada ya miaka saba kupita Yohana
alipelekwa Hospitali Teule ya Ikonda wilayani Makete kupata huduma za
tatizo lake. Alifanikiwa kupata msaada wa baiskeli ya magurudumu, ambayo
aliitumia kwa miaka mitano.
Kwa sasa baiskeli hiyo haifanyi kazi
kutokana na watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi kuiba matairi na vyombo
muhimu vinavyoiwezesha baiskeli hiyo kufanya kazi.
Pamoja na kupewa baiskeli hiyo na
wasamaria wema, Yohana anakiri pia kuchongewa viatu na hospitali hiyo
ambavyo vinamuwezesha angalau kutembea umbali mfupi.
Kutokana na ulemavu huu wa kimiujiza,
Yohana anakiri ndoto zake za maisha hazijatimia mpaka leo na inawezekana
zikawa zimepotea kabisa.
Mipango yake
Alipinga mambo mengi yakiwemo kusoma na
hata kufungua miradi ya maendeleo. Sasa ni kama anaona haiwezekani tena
kwa sababu hana uwezo thabiti wa kufanya kazi; ukizingatia ni kijijini
ambako kazi kubwa inayotegemewa kiuchumi ni kilimo cha jembe la mkono.
Ulemavu huo umesababisha ashindwe kuoa,
kwani anasema katika ulimwengu wa sasa ni ngumu kuoana na mtu kama huna
uwezo wa kumhudumia.
Anasema ilikuwa ni ngumu kwa ndugu
kuamini kinachotokea lakini anawashukuru wasamaria wema walioendelea
kumhudumia mpaka pale alipoikubali hali yake na kuanza kuishi katika huo
mfumo mpya wa maisha.
Kwa sasa Yohana anaishi na dada yake
mkubwa aitwaye Lucy Nkwera akimsaidia kwa mahitaji ya kila siku ikiwemo
chakula na huduma za usafi na usalama kwa jumla.
Akisimulia kwa hisia, Yohana anakumbuka
jinsi alivyokuwa katika hali ya uzima wa miguu na kujitegemea, kwamba
anashangaa sana kuona leo amekuwa ni mtu wa kuomba msaada; kwa sasa
msaada wake mkubwa ni dada yake huyo.
Lucy anasema, “Maisha ni magumu sana kwa kuwa anatakiwa kuwa karibu naye, kwani hakuna mwingine wa kumsaidia.”
Mbali na kupata huo ulemavu wa miguu, Yohana anaumwa ugonjwa wa kifafa, ambao nao aliupata baada ya kukatika miguu.
Ugonjwa huu unamfanya kupoteza fahamu mara kwa mara kitendo ambacho ni hatari kwa afya na maisha yake.
Anamshukuru Lucy kwa kuendelea
kumhudumia kwa sababu kwa mazingira ya kawaida ni wachache wenye moyo wa
huruma kiasi hicho, hasa kumhudumia mgonjwa ambaye hatarajii kupona leo
hata kesho.
Anashukuru pia ndugu zake kutoka maeneo mengine akisema kuwa nao wamekuwa wakija kumtaka hali na kumletea vyakula.
Anaishukuru Serikali ya Kijiji cha Ludewa anachoishi, kwa kumkumbuka na kumhudumia kwa kadiri wanavyoweza.
Anasema kama Serikali na ndugu
wasingekuwa wanamsaidia, huenda hali yake ingekuwa ngumu zaidi na ilivyo
sasa kwani kwa jumla afya yake ni dhaifu.
Ushauri wake
Yohana anawaomba watu kuachana na tabia za kunyanyapaa walemavu.Anasema baada ya kuwa na ulemavu, kuna marafiki zake walimtenga.
“Inauma sana kuona kumbe wengine ni
marafiki wa wakati wa raha...Ukiwa na matatizo wanakukimbia, hii tabia
si nzuri, ni lazima tuwe na moyo wa kusaidiana wakati wote,” anasema
Yohana.
Anaongeza kuwa hata yeye hakupenda kuwa
katika hali ambayo anayo sasa. Ndiyo kusema kwamba yeyote anaweza
kupatwa na lolote kabla ya hajafa, tusinyanyasane.
chanzo-MWANANCHI

No comments:
Post a Comment