Wasanii waliotangulia mbele za haki kwa kufuatana ni Adam Kuambiana, Sheila Leo Haule ‘Recho’, George Otieno ‘Tyson’ na Said Ngamba ‘Mzee Small’.
Misiba hiyo imetokea ikiwa ni baada ya utabiri wa mtabiri maarufu Bongo, Maalim Hassan Hussein Yahya ambaye aliwatabiria vifo wasanii katika kipindi cha mwaka mmoja wa utabiri.
MASTAA KANISANI
Dawati la Risasi Mchanganyiko lilinasa habari kutoka katika chanzo chake, kilichoeleza kuwa Kanisa la Nchi ya Ahadi lilipanga kufanya maombi maalum, Jumapili ya Juni 15, mwaka huu kwa wasanii wa filamu Bongo kwa lengo la kuangamiza roho wa mauti anayekatisha ndoto zao.
Pekupeku za gazeti hili zilionyesha kuwa, uongozi wa kanisa hilo ulisambaza ujumbe kwa wasanii mbalimbali wa filamu Bongo ukiwataka wafike kanisani hapo bila kukosa kwa ajili ya maombi.
“Wametoa tangazo hadi redioni, wamesisitiza wasanii waende kwa wingi ili wakaombewe. Wachungaji wa hilo kanisa wapo kwenye funga na maombi kwa ajili ya mambo mbalimbali yanayohusu nchi ikiwemo misiba ya wasanii wa filamu ambayo inatishia kiukweli,” kilisema chanzo hicho.
MAPAPARAZI KANISANI
Timu ya gazeti hili ikiambatana na wenzao wa Global TV walitinga kanisani hapo Jumapili iliyopita mishale ya saa tano asubuhi ambapo ilikuta kanisa likiwa limefurika waumini na baadhi ya wasanii wa filamu huku wengi wakiwa ni wale wanaochipukia.
MWAKIFWAMBA, DOTNATHA WAWEKEWA MIKONO
Katika hali ya kushangaza sana, mastaa waliohudhuria walikuwa wawili tu; Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’, Simon Mwakifwamba na Illuminata Posh ‘Dotnatha’ ambao waliwekewa mikono na wachungaji waliokuwepo kwenye ibada hiyo.
Baadhi ya wachungaji waliowaombea mastaa hao ni Mchungaji Harris Kapiga na Mchungaji Mbeyela ambaye ni mume wa mwimbaji wa muziki wa Injili nchini, Upendo Nkone.
MCHUNGAJI ANENA
Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Harris Kapiga akizungumza na waandishi wetu baada ya ibada hiyo ya kuharibu roho wa mauti alisema, wasanii ni nembo ya taifa ndiyo maana wameona ni vyema kupambana na roho wa giza anayesababisha vifo miongoni mwao.
“Roho wa kifo ni kitu kamili. Anaishi katika ulimwengu wa giza, dawa yake ni maombi tu. Sisi kama kanisa tumeona ni vizuri kumlilia Mungu kwa ajili ya wasanii wetu, kwa maombi tuliyofanya, hakuna msanii mwingine atakayekufa katika kipindi hiki,” alisema Mchungaji Kapiga na kuongeza:
“Hatujali uchache wao, lakini tunaamini kuwa huko walipo watapokea uponyaji. Yaani hata kama kusingekuwepo na msanii yeyote, ibada ingeendelea kama kawaida. Kwa sasa nasema, wasanii wasiwe na wasiwasi juu ya roho wa mauti.”
Simon Mwakifwamba, Bahati Bukuku na Dotnata wakicheza wimbo wa Dunia Haina Huruma ulioimbwa na Bahati Bukuku.
MWAKIFWAMBA ANENA
Rais wa TAFF, Mwakifwamba alipoulizwa kuhusu uchache wa wasanii waliohudhuria ibadani hapo alisema: “Imani imekosekana kwa wasanii, maana kama wangekuwa nayo leo wengefurika hapa, lakini siwezi kuisemea nafsi ya mtu kwa maana kila mtu ana imani yake.
“Mimi nimefarijika sana na nina imani huyu pepo wa vifo anayetuandama hatakuwa na nafasi tena kwetu.”
Rais wa TAFF, Mwakifwamba alipoulizwa kuhusu uchache wa wasanii waliohudhuria ibadani hapo alisema: “Imani imekosekana kwa wasanii, maana kama wangekuwa nayo leo wengefurika hapa, lakini siwezi kuisemea nafsi ya mtu kwa maana kila mtu ana imani yake.
“Mimi nimefarijika sana na nina imani huyu pepo wa vifo anayetuandama hatakuwa na nafasi tena kwetu.”
Mchungaji Harris Kapiga akiongoza ibada ya maombezi Katika Kanisa la Nchi ya Ahadi, jijini Dar es Salaam.
DOTNATHA ACHARUKA“Mimi nawashangaa wasanii wenzangu kwa kweli, hawana imani na mambo ya kiroho. Kiukweli ushirikika ni tatizo sana kwa wasanii. Leo kama wangekuja tukajumuika pamoja lingekuwa jambo zuri sana.
“Wasanii tupo kwenye hatari kubwa, lakini hii inatokana na wasanii wengi kujikita kwenye mambo ya kishirikina zaidi ya kumwabudu Mungu wa kweli. Nawashauri tumrudieni Mungu tutapona,” alisema Dotnatha.
TURUDI KWA MTABIRI
Hata hivyo, mnajimu maarufu nchini, Maalim Hassan Hussein Yahya hivi karibuni alisisitiza kuwa, vifo kwa wasanii nchini vitaendelea hadi mwaka wa kiutabiri utakapomalizika hapo Aprili, mwakani.
“Huu ni utabiri na kama nilivyosema, utabiri ni mambo ya mahesabu ya kinajimu. Hakuna kitakachobadilika, vifo kwa wasanii, tena siyo Tanzania pekee - duniani vitaendelea hadi mwezi Aprili mwakani,” alisisitiza Maalim Hassan.
MTABIRI MWINGINE
Baada ya kifo cha Mzee Small aliibuka mtabiri mwingine, aliyejitambulisha kuwa ni Nabii wa Kanisa la Ufufuo lililopo Buza, jijini Dar es Salaam, Yaspi Paul Bendera ambaye amekazia kuwa vifo kwa wasanii wa filamu za Kibongo vitaendelea.
Akizungumza bila hofu, Nabii Bendera alisema: “Watakufa wasanii 20 ndani ya mwezi huu (Juni). Huu si utani, ni maono.”
Bendera aliwataka wasanii wafike kanisani kwake ili awaombee na kuwapaka mafuta matakatifu yatakayowakinga na vifo.
TUJIKUMBUSHE
Katika misa ya kumuombea marehemu Tyson iliyofanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar, Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Inuka Uangaze, Buldozer Mwamposa aliwaombea wasanii wote akisema kuwa hakuna msanii atakayekufa tena.
Hata hivyo, licha ya kauli hiyo, siku chache baadaye mkongwe kwenye sanaa ya maigizo, marehemu Mzee Small alitangulia mbele za haki.
KUTOKA KWA MHARIRI
Sisi kama gazeti, hatuko upande wowote katika utabiri unaotangazwa na wanajimu na viongozi mbalimbali wa dini nchini lakini tupo pamoja na wafiwa katika kipindi hiki kigumu huku tukiamini kuwa kifo ni ahadi kutoka kwa Mungu.
Maneno yaliyotumika kwenye picha za wasanii picha ya kwanza, si halisi bali ni kama wanafikiri tu!
No comments:
Post a Comment