UNAPOMUOMBA MSAMAHA MPENZI WAKO BASI, UAMBATANE NA MABADILIKO YA VITENDO

Wiki hii kama kawaida nazungumzia mada inayogusa maisha yetu ya kimapenzi, si unajua bila mapenzi hakuna maisha! Huo ndiyo ukweli, huwezi kuishi kama jiwe au mti. Raha ya maisha ni kuwa na mpenzi wa kumpenda na yeye akakupenda kiukweli na siyo kuigiza kama ilivyo kwa baadhi ya watu.

 
Kwa wale walio katika mapenzi matamu na ya kweli watakubaliana na mimi kuwa mapenzi yenye amani na masikilizano ni kama ‘kapepo’ kadogo ndani ya ulimwengu huu mkubwa uliojaa vituko!
Wakati wengine wakiishi kwa raha katika maisha yao ya kimapenzi, wapo wanaoishi na wapenzi wao huku mioyo yao ikiwa imesinyaa!  Kila siku ni karaha na vituko vya makusudi kutoka kwa wapenzi wao japo wanawapenda sana na kuonesha mapenzi yao yote.
Kila siku ni maumivu na simanzi ya moyo isiyojulikana hatima yake.
Lakini pamoja na karaha, vituko na dharau zinazofanywa na wale tuwapendao, bado kuna ambao wamejaaliwa mioyo ya uvumilivu. Hawa ni wale wanaoamini ule msemo usemao, subira yavuta heri. Yaani wanaamini ipo siku wapenzi wao watabadilika na maisha yatakuwa matamu.
Ni kweli kuna wanaofanikiwa katika hili lakini wapo ambao uvumilivu wao unapitiliza. Ndugu zangu, kila kitu kina kikomo, kama umevumilia kwa muda mrefu lakini ukaona hakuna mabadiliko, uamuzi sahihi ni ‘kusitisha safari’.
Lakini kama una moyo wa chuma na huumizwi na yale mabaya anayokufanyia mpenzi wako, hakuna anayeweza kukulazimisha umuache. Watu watakuangalia na kuishia kukuonea huruma tu.
Labda unaweza kujiuliza ni kwa nini baadhi wanavumilia mabaya wanayotendewa na wapenzi wao? Iko hivi, yawezekana anayevumilia anahisi huyo aliyenaye ndiye mtu sahihi na anaamini akimuacha atampata mwenye mateso zaidi, hivyo anaona amvumilie huyo aliyemzoea.
Lakini wengine ni ulimbukeni tu, yaani wao wanahisi hayo ndiyo maisha. Kutukanwa, kupigwa, kusalitiwa na kufanyiwa mambo mengine ya namna hiyo ni sehemu ya maisha. Yaani wanaamini si wao tu bali hata kwa wengine ni hivyohivyo. Mh!
Lakini sasa kuna hili suala la kukosewa na mpenzi wako kisha akakuomba samahani. Hili katika mapenzi linakubalika kabisa kwani kila siku tunakoseana na samahani ndilo neno linaloweza kurudisha amani katika penzi.

 
Kuna watu ni wagumu sana kuomba msamaha. Yaani wanajua wamekosa lakini wanaona kuomba msamaha ni kujishusha. Hii ni mbaya sana na inaweza kusababisha kupunguza mapenzi kati ya wawili waliotokea kupendana.
Pia kuna ambao ni wagumu kusamehe. Yaani mpenzi wake kafanya kosa kwa bahati mbaya na anagundua amekosea lakini akiomba msamaha, hasamehewi. Hili nalo ni tatizo!
Ila sasa kuna watu ambao kila siku ni samahani tu. Wapo ambao kila siku wanakosewa na wapenzi wao na kuishia kuombwa msamaha.
Hili kimsingi ni jambo linaloweza kuleta picha ya tofauti.
Tunachojua ni kwamba, unafanya kosa leo, unaomba msamaha na kutorudia tena kosa. Lakini kama leo unamsaliti mwenzako, anakusamahe, kesho tena unasaliti, kwa kuwa anakupenda anakusamehe, keshokutwa tena unarudia kosa lilelile, katika mazingira hayo ni kweli unastahili kuendelea kusamehe?
Sidhani kama inakuja! Kurudia makosa yaleyale kwa kutarajia kuwa utaomba msamaha na kusamehewa ni kuonesha kwamba unamdharau mwenzio na kimsingi kama utakuwa ni mtu wa ‘am sorry dear’ kila siku na hubadiliki, hiyo ‘am sorry’ yako haitakuwa na faida.
Ninachoweza kusema ni kwamba, kama huyo uliyenaye unampenda kwa dhati, anaweza kukukosea mara nyingi kwa makosa mbalimbali na ukaendelea kumsamehe bila kuchoka kwa kuwa unampenda na hauko tayari kumkosa kwa makosa yanayosameheka.
Lakini kama mpenzi wako atakukosea makosa mawili-matatu kisha ukafanya uamuzi wa kumuacha, utakuwa unadhihirisha kwamba, hukuwa na mapenzi ya dhati kwake na ndiyo maana kakukosea mara moja au mbili, ukaona ndiyo mwanya wa kumpiga kibuti.
Tujenge utamaduni wa kusameheana kwani hakuna aliyekamilika kwa asilimia 100 na ndiyo maana kila siku tunakoseana.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger