MTOTO Mariam Shabani (5) aishiye Bunju A Zone Kizota
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambaye alizaliwa akiwa mzima,
amekumbwa na ugonjwa wa ajabu unaowashangaza wazazi wake.
Mzazi wa mtoto huyo, Idd Shaban aliwaambia waandishi wetu kuwa
mwanaye akiwa mchanga alisadikika kuwa na matatizo ya ubongo lakini
ukuaji wake ulikuwa mzuri kama wanavyokuwa watoto wengine.
HALI ILIPOANZA KUBADILIKA
Akifafanua zaidi
Shaban alisema: “Alipofika umri wa miaka miwili hali ilibadilika akawa
mtu wa kulala tu na mpaka sasa hawezi kufanya chochote.
“Baada ya
kupata hayo matatizo tuliamua kumpeleka Hospitali ya CCBRT iliyopo
Msasani Dar kwa ajili ya matibabu zaidi lakini ilishindikana na
madaktari walisema tuwe tunampeleka katika tawi la Hospitali ya CCBRT
lililopo Tegeta kwa ajili ya mazoezi kwa ahadi kuwa hali yake itakuwa
sawa.
ASHINDWA KUTEMBEA, KUONGEA
“Tuliendelea na
mazoezi katika Hospitali ya Tegeta lakini hali ilizidi kuwa mbaya
kabisa kwani Mariam akawa ajiwezi kwa chochote si kutembea wala kuongea,
akawa ni mtu wa kulala muda wote, mbaya zaidi mpaka sasa hawajui kama
anasikia au la sababu hata tukimsemesha haonyeshi ushirikiano.
“Kwa kweli mwanangu anapata wakati mgumu sana kwani hata akiumwa
hatuwezi kujua mpaka alie au awe na joto kali, kuna siku alianguka
kutoka kitandani na kuvunjika mguu kiukweli tulipata tabu kumtibu
kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu, tulijitahidi akapona mguu kwa
pesa za kududunduliza.
ALIKUWA ANAONGEA NA KUCHEKA
“Naumia sana kuona
mwanangu yupo katika hali mbaya wakati alizaliwa akiwa mzima asiye na
kasoro, alikuwa anaongea, anacheka pia aliwahi kutambaa na kutembea
katika ukuaji wake utotoni.
“Nakiri kuwa tuliambiwa ana mtindio wa
ubongo, huenda hiyo hali ilichelewa kujitokeza mpaka baada ya miaka
miwili ndipo hali hii ikajitokeza.
NATAMANI AWE AKIENDA SHULE
“Sijui hatima ya
mwanangu, natamani kuona binti yangu anakwenda shule kama watoto wengine
hata kama siyo shule za kawaida basi za watoto wenye mtindio wa ubongo
japo uwezo kifedha sina.
“Mimi ni mjenzi na nina kipato kidogo sana,
nawaomba wasamaria wema, Watanzania wenzangu wanisaidie fedha za
matibabu na kibaiskeli cha kumbebea kwa sababu tumemtengenezea kiti cha
mbao ambacho kinamuumiza,” alisema Shaban.
Yeyote aliyeguswa na habari ya kusikitisha ya mtoto Mariam awasiliane na mzazi wake kwa simu namba 0718 848 895.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment