MWANZILISHI WA KANISA AJITANGAZA KUWA YEYE NI YESU NA WATU WAKAMUAMINI, MUONE HAPA

SHETANI bado anazidi kuwasakama Wakristo duniani. Hii ni baada ya mkazi wa Kijiji cha Alvaro Thesiss, Santa Catarina nchini Brazil, Mtume Inri Cristo (66) mwanzilishi wa Kanisa la Waraka Mweusi (Suprema Ordem Universal da Santíssima Trindade ‘Soust’), miaka 35 iliyopita kujitangaza kuwa yeye ni Yesu Kristo amerudi kuja kuwaokoa wanadamu baada ya kusubiriwa kwa miaka mingi.
Mtume Inri Cristo 'Yesu feki' akifanya maombi pembeni ni wafuasi wake.
Cristo kwa sasa anaitikisa dunia kwa kuwahubiria maelfu ya watu wa madhehebu ya Kikristo sehemu mbalimbali duniani huku akijiita Yesu Kristo wa Nazareti.
MAHUBIRI YAKE YATIKISA
Mei, 2013, Cristo alitua katika Jiji la Sao Paulo nchini humo na kuwaombea Wakristo, wakiwemo makahaba. Alipokelewa kwa heshima zote huku akijitangaza kuwa hakuna atayekuja duniani kuwakomboa wanadamu zaidi yake.

Mtume Inri Cristo 'Yesu feki' akimuombea muumini.
Alihubiri kuwa kwa kila kiumbe mwenye matarajio ya kuingia kwenye ufalme wa mbinguni yeye ndiye njia ya kweli na uzima.
YESU FEKI AKUTANA NA MAGUMU
Septemba, 2013, mzee huyo alitua kwenye Jiji la Rio de Jeneiro kwa lengo hilohilo lakini alijikuta akishambuliwa vikali huku Wakristo wa jiji hilo wakimtupia lawama kuwa ni mhubiri feki aliyevaa ngozi ya kondoo kujipatia kipato kinyume na utaratibu wa makanisa mengine ya Kikristo nchini Brazil.

AITWA MHUBIRI PUNDA
Akiwa katika harakati zake za kuwavuta waumini wa makanisa ya Kikristo katika Jiji ya Sao Paulo wakati wa Sikukuu ya Krismasi, mwaka jana, mhubiri huyo feki alishambuliwa tena na waumini wa eneo hilo ambao walikusanyika kwenye mkesha wa sikukuu hiyo.

Yesu feki akiwa kwenye kiti chake.
Baadhi ya waumini walimzomea kwa mahubiri yake huku wakisema hayana tofauti na punda aliyebebeshwa mzigo mzito na kushindwa kuutua.
Hata hivyo, Yesu feki huyo aliwajibu waumini hao kwamba hawajui walitendalo kwani yeye ndiye Yesu wa kweli aliyetumwa na Mungu kuja duniani kuwaokoa wanadamu.
“Mimi sijali maneno yao, wameniita punda, eti mahubiri yangu hayana tofauti na punda aliyebebeshwa mzigo mzito hivyo hawezi kujinasua siku zote ataishia kutapatapa, mimi nimetumwa na Mungu,” alisema Cristo.
Yesu feki akiwa na wapambe wake.
ANASWA NA KASHFA YA UTAPELI  
Akiwa amejiamini na kujijengea heshima kubwa kwa waumini wake, Januari Mosi mwaka huu, mhubiri huyo alishambuliwa kwa maneno na watu wasiojulikana kwa kusambaza nyaraka za wazi zilizokuwa zimeandikwa kuwa yeye ni tapeli mkubwa kwani anadanganya watu ili kujipatia fedha.

Kitendo hicho kilimpunguzia umaarufu kwani alikuwa ameweka utaratibu kwa waumini wake kulipa fungu la kumi kwa kila pato, alijiweka zaidi kwa wafanyabiashara wakubwa nchini Brazil huku akiwaonya kuwa bila yeye hawawezi kufanikiwa kimaisha.
HISTORIA YAKE KIDUNIA
Cristo aliyezaliwa Machi 22, 1948 mwenye wafuasi wengi katika kanisa lake, amewahi kutembelea nchi nyingi duniani akieneza uzushi huo kwamba yeye ni Yesu Kristo.

Yesu feki akiomba.
Amewahi kufukuzwa kwenye baadhi ya nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini zikiwemo Uingereza, Venezuela, Peru, Marekani na Ufaransa ambako alitaka kuanzisha makanisa. Pia ameshawahi kuwekwa ndani mara 40 nchini mwake kutokana na kujitangaza kuwa yeye ni Yesu na kuvuta watu wengi.
Katika nchi yake, Cristo amefanikiwa kuwafanya waumini wake waishi pamoja naye kwenye makazi jirani na kanisa lake la Santa Catarina.
Wazazi wa mzee huyo, baba Wilhelm na mama Magdalena Thais ni Wakatoliki wenye asili ya nchini Ujerumani.

Tangu mwaka 1979, Cristo amesafiri zaidi ya nchi 27  duniani kote akieneza neno lake huku akisema yeye ni Mfalme wa Wayahudi aliyerejea duniani kwa mara ya pili. Pia husema eneo la kanisa lake ni Yerusalemu mpya.
...Akiwaombea waumini.
MAVAZI YAKE
Mara zote, Cristo huvaa kanzu nyeupe na viatu vya ‘makubazi’ huku kichwani akiwa na mduara wenye kuashiria taji la miiba alilovalishwa Yesu wa kweli.

ETI ALIISIKIA SAUTI YA MUNGU
Katika mahojiano yake na baadhi ya redio nchini humo, mhubiri huyo amekuwa akisema tangu utotoni mwake alikuwa akiifuata sauti ya Mungu ambayo ilikuwa ikisema: “Mimi ni Baba yako. Mungu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo.”

ANA MPANGO WA KUTEMBELEA AFRIKA
Inasemekana wakati wowote mwaka huu, Cristo atatembelea nchi mbalimbali za Bara la Afrika kwa lengo la kuvuta wafuasi wengi.

Nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini, Tanzania, Togo, Mali, Misri, Angola, Nigeria, Burkina Faso na Zaire zinadaiwa kuwepo kwenye ratiba ya ‘Yesu’ huyo.
VIONGOZI WA DINI NCHINI WAMKEMEA
Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wachungaji na maaskofu wa Tanzania kusikia wanamzungumziaje mhubiri huyo feki.

MCHUNGAJI MTIKILA
Mchungaji wa Kanisa la Full Salvation Church la jijini Dar es Salaam, Christopher Mtikila alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusiana na sakata hilo, alisema:

“Huyo ni shetani mkubwa, akija Tanzania hatutaki kumwona kwani anakuja kuwavuruga waumini wetu.”
ZAKARIA KAKOBE
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship lenye makao yake makuu kwenye Jiji la Dar es Salaam, Zakaria Kakobe naye alikuwa na haya ya kusema:
“Huyo akija Dar anatakiwa tumuombee ili mapepo yamtoke, awe mzima na  amsifu Mungu.”

MZEE WA UPAKO
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi nalo la jijini Dar, Lusekelo Antony ‘Mzee wa Upako’ alisema utabiri wa Yesu kuwa nyakati za mwisho wengi watajitokeza wakidai ni Kristo umetimia.

“Hizi ni nyakati za mwisho kweli. Yesu alisema watatokea manabii wengi wakisema wao ndiyo Kristo, ndiyo hao sasa. Hataweza kuushinda utawala wa Mungu aliye hai,” alisema Mzee wa Upako.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger