Mwanamuziki Mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Henry Mkanyia akiwa ndani ya ofisi za Global Publishers.
Akizungumza na waandishi wa Kampuni ya Global Publishers
inayochapisha gazeti hili, Championi, Amani, Ijumaa, Risasi na Ijumaa
Wikienda, Mkanyia alisema muziki wa dansi na ule wa asili ni moja ya
silaha ambayo inaweza kutumika kuongeza watalii na kuitanga nchi
kimataifa.Katika mahojiano hayo ambayo yamerushwa na Global TV On line, Mkanyia ambaye ni mpiga gitaa maarufu wa Bendi ya JKT ‘Kimbunga’ na baadaye Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’, alisema ipo haja nchi kugeukia upande huo ambao anaamini kuna ujumbe mzito unaotolewa kwa watu kupitia mashairi ya nyimbo mbalimbali.
Baadhi ya mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwandishi: Unaweza kutupa historia yako kwa kifupi?
Mkanyia: Nilianza muziki nikiwa mdogo sana. Nilikuwa darasa la tatu mwaka 1963 kwa kupiga ngoma za asili za Kimakua na Kiyao katika Kijiji cha Mkarango, Masasi. Baadaye nilijitengenezea gitaa na nilipomaliza shule ya msingi nikaanzisha bendi yangu. Lakini katika kutaka maendeleo zaidi nikajiunga na bendi ya Masasi ambayo ilikuwa inatumia magitaa ya umeme.
Baadaye nilijiunga na Bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa, Wana Kimbunga lakini nikatua rasmi DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ mwaka 1991.
Mwandishi: Ukiwa Sikinde mlikuwa wanamuziki wengi wapiga gitaa la solo kama wewe, utaratibu ulikuwaje wakati wa kutunga wimbo?
Mkanyia: Wimbo unapoletwa sisi wapiga magitaa tulikuwa tunagawana kazi, nani apige nini. Ni kweli nilikuwa na wapigaji mahiri wa magitaa kama vile Abel Baltazar, Joseph Mulenga, Abdallah Gama na wengine wengi lakini Abel mara nyingi alikuwa nje ya sehemu yetu ya mazoezi kwa sababu alikuwa meneja wa bendi, hivyo muda mwingi hakuwa mazoezini.
Mwandishi: Ukiwa Sikinde uliwahi kusafiri nje ya nchi, je ni wapi na mlijifunza nini huko?
Mkanyia: Tulisafiri nchi nyingi sana za Ulaya kama vile Ujerumani, Holland, Swaziland, Ubelgiji, Austria nakadhalika, nilikuwa napiga solo gitaa na gitaa la pili (second solo) bila wasiwasi kwa sababu namudu magitaa yote.
Nilichojifunza kule ni kwamba huko Ulaya wanapenda sana kusikia muziki wa Kiafrika, hasa wa Kitanzania. Walifurahi sana walipotuona na wengine wakavutiwa kutaka kuja nchini kutalii, hivyo nikagundua kuwa muziki wa Kitanzania unaweza kutumika kuitangaza nchi kimataifa na kuongeza watalii nchini. Nilifarijika kukuta wapo Wazungu waliowahi kufanya kazi Tanzania na wanajua Kiswahili kwa ufasaha.
Mwandishi: Ukiwa Sikinde mlikuwa na mwalimu King Michael Enock, unamzungumziaje mwanamuziki huyo? Je, uliwahi kutunga wimbo Mlimani Park?
Mkanyia: Alikuwa mwanamuziki mahiri, mwalimu wa magitaa, sauti na hata tungo. Sina wa kumfananisha kwa sasa. Sikinde nilitunga wimbo mmoja tu uitwao Nyerere Baba, ukweli ni kwamba sikujikita katika utunzi.
Mwandishi: Tunajua Sikinde uliiacha, je ni kwa nini na sasa upo wapi kimuziki?
Mkanyia: Sikinde niliagana nao rasmi na kujing’atua mwaka 1994, niliitumikia miaka 14 nikaamua kuanzisha bendi yangu ya Tanzania Brothers nikiwa na wanamuziki wengine wa Sikinde kama vile Tino Masinge, Kalamazoo, Kassim Rashidi na wengine wengi lakini bendi haikudumu kutokana na uchakavu wa vyombo.
Mwandishi: Ikawaje baada ya hapo?
Mkanyia: Sikukata tamaa, nilijikusanya baadaye mwaka 1995 nilishirikiana na mwanangu Leo Mkanyia kuanzisha bendi inaitwa Swahili Blues ambayo sasa ina miaka minne na tunapiga kwa mkataba katika Hoteli ya Serena katikati ya Jiji la Dar es Salaam kila Ijumaa kuanzia saa moja usiku, siku nyingine katikati ya wiki tunaweza kukodishwa kwenye sherehe mbalimbali pale hotelini au nje.
Mwandishi: Unazungumziaje muziki wa Bongo Fleva na hasa mwanamuziki Diamond anayeng’aa sana nchini?
Mkanyia: Muziki wao ni mzuri nikiangalia ujumbe japokuwa wamezidisha kuzungumzia mapenzi. Nawashauri wajifunze ala za muziki. Diamond ni mwimbaji mzuri sana, ‘anatisha’, na ana sauti nzuri lakini kasoro yake ni hiyo ya kutojua ala za muziki. Nawashauri wasipuuze hilo.
Mwandishi: Kwa nini siku hizi muziki wa dansi hupigwa sana kwenye baa kuliko ukumbini?
Mkanyia: Jibu ni rahisi, kwamba kwenye ukumbi kuna gharama kubwa. Huwezi kujaza watu bila kujitangaza kwa kutumia magazeti, redio na runinga. Kufanya hivyo kunahitaji gharama kubwa lakini hotelini huna gharama hizo, lakini lengo la muziki ni kufikisha ujumbe na haijalishi unafikisha kwa kupiga wapi.
No comments:
Post a Comment