Nawatakia heri ndugu zangu Waislam popote duniani ambao mpo katika
funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mwenyezi Mungu awajalie, maana
mnatimiza moja ya nguzo muhimu katika imani na Inshallah Mola awafanyie
wepesi muweze kutekeleza vyema.
Sasa
turejee katika mada yetu ambayo naamini itawafumbua wengi. Watu wote
wana umuhimu wa kuingia kwenye ndoa lakini kuna tofauti kidogo, kwamba
mwanamke anasubiri kufuatwa na mwanaume, wakati mwanaume anaamua
kumfuata mwanamke anayemtaka kwa wakati wake.
Wanawake wa ‘mjini’
huwa hawakubaliani na hili, kutokana na huu utandawazi unaohubiriwa siku
hizi ikiwa ni pamoja na kampeni za usawa zinazotetewa na wanaharakati
wa kijinsia.
Tuyaache hayo, hoja kubwa ya msingi hapa ni je, umempa sababu
mwanaume wako za kumfanya afikirie kukuoa? Ikumbukwe kwamba, hapa
nazungumza na wanawake ambao tayari wapo katika uhusiano, lakini wenzi
wao hawana habari kabisa na mambo ya ndoa.
Inawezekana anawaza kuhusu ndoa na anafikiria kuhusu kuoa lakini
mambo yako ndiyo yanamshangaza. Ipo staili au mtindo unaompasa mwanamke
awe ili kumpa sababu mwanaume ya kuamua kumuoa.
Kumbuka kipindi cha uchumba ni wakati ambao mwanaume hutumia muda
mwingi kumsoma mwanamke wake, kuangalia ni kwa namna gani anaweza
kupanga maisha yake na mwanamke sahihi.
Maana yake ni kwamba,
anaweza kuwa na wewe lakini tabia zako, mwenendo wako ukamfanya ahisi
kuwa si mwanamke sahihi wa kuingia kwenye ndoa. Jambo kubwa unatakiwa
kufahamu; si kila mwanamke anaweza kuwa mke.
Zipo
tabia zinazompasa mke kuwa. Lakini pia kuna mambo ambayo yakifanywa na
mtu ambaye hana mpango wa kuolewa na hayupo kwenye ndoa, yanakubalika.
Je, unajua unapaswa kuwa vipi ili uolewe? Ndugu zangu, kila kitu kina
taratibu zake. Si mada ya wanawake tu, hata wanaume wanaweza kujifunza
kitu kupitia mada hii. Kwa kuangalia tabia zifuatazo itakuwa rahisi kwao
kufanya uchaguzi wa mke aliye sahihi.
MAKUNDI
Mwanaume anapenda kuwa na mke mwenye staha, ambaye hana
tabia za hovyo. Kuwa na makundi ya ‘mashangingi’ ni alama ya kwanza
kabisa kuwa unapenda au tayari una tabia za kishangingi.
Wanaume wengi hawapendi kabisa wanawake wenye tabia za hovyo, wenye kampani ambazo si nzuri.
Lakini yawezekana jamaa alishakuambia juu ya kilio chake hiki, lakini
wewe umekuwa kama umeweka pamba masikioni mwako, hili ni tatizo.
Linda heshima yako, kaa mbali na makundi hatari, ili umfanye mpenzi
wako akuone mwanamke thabiti ambaye huigi, hushabikii na wala huna tabia
mbaya. Utaonesha hili kwa kukaa mbali na makundi ya wanawake hatari!
MAVAZI NI TATIZO
Kila mtu anamjua mtu wake alivyo, mwanamke hata
wewe unamjua mpenzi wako alivyo. Sina shaka unafahamu anapenda nini na
nini anachukia. Lakini pamoja na kwamba jamaa anaweza kuwa na vitu
ambavyo vinamvutia zaidi, hata wewe kama mtoto wa kike, una mapendekezo
yako au vitu ambavyo unapenda zaidi kuvifanya!
Huzuiwi, lakini swali la msingi, mwenzi wako anapenda? Kama wewe
unapenda sana skin jeans na top inayoacha kitovu nje, yeye hapendi kwa
sababu ana nia ya kukufanya mke hapo baadaye.
Mavazi ya kuchoresha
mwili kwa mwanamke si sahihi. Sasa utakuwa mke gani ambaye hata ‘Salim’
anaona sehemu zako za faragha hadharani?
Ukiachana na chaguo la mwenzi wako, lakini lazima wewe kama mwanamke wa mtu, ujitambue! Jisitiri vyema.
Kwani kuna urembo gani wa kuvaa nguo inayoonesha mwili wako ulivyo?
Kuna burudani gani kuacha nyeti zako wazi? Unataka nani akuone ulivyo?
Mke hana sifa hiyo, sasa ili uweze kuwa na sifa hii muhimu, lazima
uzingatie sana mavazi yako.
Wiki ijayo, mada itaendelea, USIKOSE!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment