FEDHA mwanaharamu! Katika hali ya kushangaza, staa
wa filamu ambaye fedha imemtembelea kwa sasa, Kajala Masanja ‘K’
amenaswa akimwaga fedha kama amechanganyikiwa mbele ya kadamnasi, Risasi
Mchanganyiko linakupa mchapo kamili.
Staa wa filamu, Kajala Masanja ‘K’ akiwatunza wakali kutoka Yamoto Band.
Tukio hilo lililowaacha watu midomo wazi lilitokea hivi karibuni
katika Viwanja vya Leaders Club Kinondoni jijini Dar, kulipokuwa na
uzinduzi wa filamu ya Mateso Yangu Ughaibuni ambapo muigizaji huyo
alionesha jeuri ya fedha baada ya kupagawishwa na sebene la Yamoto Band.
ALIINGIA NA WAPAMBE
Awali, paparazi wetu
alimshuhudia Kajala akitinga viwanjani hapo akiwa ameongozana na wapambe
takriban 15 na kwenda kukaa katika meza moja ambapo mhudumu
aliwasikiliza kujua wanachokunywa.
VINYWAJI VYAAGIZWA NJE
Kutokana na uzinduzi huo kutokuwa na pombe, K aliamuru kila mtu aletewe
kile anachokihitaji halafu bili yote apelekewe yeye, Mama la Mama kama
wanavyowaita watoto wa mjini.
“Waletee hawa vinywaji wanavyojisikia kunywa pia wasikilize meza ile pale kisha bili niletee mimi,” alisikika Kajala.
Mama wa Wamama 'Kajala' akirudi kukaa mara baada ya kuwatunza wakali wa Yamoto Band.
MINONG’ONO YAMTIA WAZIMU
Baada ya kauli ile
wafuatiliaji wa mambo ya watu hasa wakienda shughulini wakaanza kutoa
minong’ono kuwa hata iweje bado Kajala hajafikia uchezeaji wa fedha kama
alivyokuwa shosti wake wa ‘long time’, Wema Sepetu aliyepewa taito ya
Madam kutokana na kujua kuzitumbua fedha.
“Kwani kuagizia watu vinywaji ndiyo
kuonyesha kufuru au jeuri ya fedha, angalia wahudumu wanavyogawa
vinywaji kwa kusuasua, unafikiri angekuwa Madam (Wema) angekubali hata
akae muda wote asiende kutunza thubutu, chezea Madame (Madam) wewe,”
alisikika mualikwa mmoja.
Kajala akiserebuka na Mwanyekiti wa Bongo Muvi, Steven Mengere 'Steve Nyerere'.
YAMOTO BAND WAMWINUA
Ndani ya muda mfupi, Kajala
akavunja ukimya baada ya bendi ya Yamoto kupiga wimbo wa Nitajuta ndipo
Kajala aliposhindwa kuvumilia na kwenda kuwamwagia fedha huku wapambe
wake wakimshangilia.
“Ndiooo mkurugenzi hivyo ndivyo ujana unavyoliwa,” kelele zilisikika kutoka katika meza waliyokuwa wameketi wapambe wake.
KAMA LAKI SITA NA USHEE
Ufukunyuzi wa paparazi wetu kwa harakaharaka, ulizihesabu fedha hizo
alizowamwagia watoto hao wa Mkubwa Fella ambapo hesabu zilionesha
zilikuwa zaidi ya shilingi laki sita.
Mama wa Wamama 'Kajala' akiwa na shosti yake 'Odama'
AKOSOLEWA
Hata hivyo kuna baadhi ya watu
walimkosoa staa huyo kwa kusema kitendo cha yeye kupata fedha kwa sasa
kinaonekana kumchanganya kiasi cha kuzimwaga pasipo kuwa na sababu ya
msingi.
“Bora angetunza kidogo na nyingine akatumia kwa vitu vya maana
likiwemo suala la kumsaidia mume wake ambaye yuko jela kwa kushindwa
kulipa faini ya shilingi mil. 200,” alisikika mdau mmoja wa filamu
ambaye hakutaka kuanikwa jina gazetini.
UZALENDO WAMSHINDA STEVE NYERERE
Kadri Kajala
alivyozidi kumwaga fedha, uzalendo ulimshinda Mwenyekiti wa Bongo Movie
Unity, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ ambapo alimfuata Kajala na kutaka
na yeye amtunze.
“Hebu kuwa na adabu, mi mkubwa wako na mimi nitunze
kwanza mambo mengine yaendelee, haiwezekani uoneshe jeuri ya fedha
kiasi hiki wakati mimi mdau nipo hapa hunipozi,” alisikika Steve
Nyerere.
AMEZIPATA WAPI FEDHA?
Baada ya vurugu zote zile
kufanyika, paparazi wetu alimvaa Kajala na kutaka kujua vyanzo vya fedha
hizo na kumuuliza kama amehongwa, akachomoa.
“Mimi sihongwi ukitegemea fedha za mwanaume huwezi kuwa na heshima
mjini, nina biashara zangu na kampuni yangu hiki ninachokitumia hapa ni
faida tu ya siku mbili tatu mimi mjasiriamali wewe,” alisema Kajala.
TUJIKUMBUSHE
Kumbukumbu zinaonesha, kipindi
ambacho Kajala na Wema walikuwa marafiki, Kajala hakuwa na fedha nyingi
lakini baada ya kutofautiana, pesa imemtembelea huku mwenzake akidaiwa
kuyumba kiuchumi.
Read more >>